Watu sita wamethibitishwa kufariki na wengine zaidi ya ishirini kujeruhiwa kufuatia mapigano makali kati ya waasi wa M23 na wapiganaji wa Wazalendo kuanzia Alhamisi Mei 15 hadi Ijumaa Mei 16, 2025, katika eneo la Bambo, jimbo la Kivu Kaskazini.
Mapigano hayo ambayo sasa yameingia siku ya tatu yamezidi kuongezeka, hali ikizidi kuwa mbaya katika eneo la Bambo, wilaya ya Rutshuru, ambako M23 bado wanashikilia ngome walizokuwa wameziteka.
Wazalendo nao wameripotiwa kuzidisha mashambulizi ya kuvizia, kwa mujibu wa kiongozi mmoja wa eneo hilo aliyewasiliana na vyombo vya habari.
Habari kutoka Bambo zinasema kuwa baada ya mapambano ya asubuhi ya Ijumaa, Wazalendo walifanikiwa kurejesha udhibiti wa Bambo, huku waasi wa M23 wakilazimika kurudi nyuma hadi Kabizo/Butare, umbali wa kilomita 2 hadi 3 kutoka Bambo.
Wananchi bado wamejificha majumbani mwao kwa hofu ya madhara ya vita. Baadhi wamekimbilia hospitali ya Bambo kujificha, na bado hawajapata fursa ya kurudi nyumbani kutokana na hali ya taharuki.
Hakuna taarifa rasmi kuhusu hali ya Kishishe, eneo ambalo M23 walikuwa wameliteka siku zilizopita. Hata hivyo, kuna madai kuwa M23 huenda hawapo tena katikati ya mji huo, na kuna uwezekano kwamba wapiganaji wa FDLR wako kwenye eneo hilo kwa sasa.
Mapigano yanazidi kuwa makali hasa katika eneo la Bwito ambako M23 wanapambana na Wazalendo pamoja na FDLR, huku ripoti zikionesha matumizi ya silaha nzito.
Kadri hali inavyozidi kuwa mbaya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hofu imezidi kwa wananchi, wengi wao wakikosa matumaini ya kurejea kwa amani na utulivu.




