Screenshot-2025-05-15-153740-768x428 (1)

Afrika Kusini Kufanya Uchunguzi wa Kijeshi Kuhusu Vifo vya Wanajeshi Wake Waliofariki Mikononi mwa M23

Naibu Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini, Bantu Holomisa, ametangaza kuwa nchi hiyo itaunda tume ya uchunguzi wa kijeshi ili kuchunguza vifo vya wanajeshi wa Afrika Kusini waliouawa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Holomisa alitoa taarifa hiyo wiki iliyopita alipokuwa akihutubia wabunge.

Afrika Kusini ni miongoni mwa nchi wanachama wa SADC zilizotuma wanajeshi katika mashariki mwa Congo kusaidia katika mapambano dhidi ya waasi wa M23.

Mnamo Januari mwaka huu, wanajeshi hao walipata kipigo kikubwa baada ya M23 kuteka jiji la Goma, na wakati huo ilithibitishwa kuwa wanajeshi 14 wa Afrika Kusini waliuawa.

Hata hivyo, ripoti nyingine zinaonyesha kuwa idadi halisi ya waliokufa huenda ni zaidi ya 50, kutokana na miili ya wanajeshi iliyopotea na haijapatikana hadi sasa, hasa kwa sababu wenz wao hawakuweza kuizoa kutoka maeneo ya mapigano.

Tangu mapema mwezi huu, SADC imeanza kuondoa wanajeshi wake kutoka DRC kupitia Rwanda, kufuatia uamuzi wa viongozi wa nchi wanachama wa kusitisha operesheni ya SAMIDRC.

Naibu Waziri Holomisa aliwaambia wabunge kuwa uchunguzi utaanza baada ya wanajeshi wote kurejea nyumbani.

Alisema:

“Baada ya kurejea kwao, Wizara kwa kushirikiana na Mkuu wa Jeshi la SANDF (Jeshi la Ulinzi la Afrika Kusini) itatoa mwelekeo kuhusu jinsi tume itakavyoundwa na kufanya kazi yake.”

Akaongeza:

“Ni Bunge lililotaka kufanyika kwa uchunguzi wa kina na wa uwazi, na tunalazimika kuheshimu ombi hilo.”

Aidha, Holomisa alisisitiza kuwa vifo vya wanajeshi havimaanishi kuwa operesheni hiyo imeshindwa, kwani kufanikiwa au kushindwa hakupimwi kwa kipimo kimoja pekee kama idadi ya vifo.

Alimalizia kwa kusema kuwa ripoti kamili itakayoshirikisha SADC, Umoja wa Mataifa, SANDF, na serikali ya DRC ndio itafichua ukweli halisi wa yaliyojiri.

Sangiza iyi nkuru

Soma Izindi Nkuru

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *