Rais Donald Trump wa Marekani amepiga marufuku raia wa mataifa 20 kuingia nchini humo, wakiwemo wa Burundi.
Trump ametangaza kuwa uamuzi huo, aliouchukua usiku uliopita, ni kwa ajili ya “kulinda nchi yake dhidi ya magaidi wa kigeni.”
Miongoni mwa nchi 19 ambazo raia wake wamezuiwa, 12 zimepigwa marufuku kabisa. Nyingi ya hizi ni nchi za Afrika.
Nchi hizo ni Afghanistan, Myanmar, Chad, Congo-Brazzaville, Guinea ya Ikweta, Eritrea, Haiti, Iran, Libya, Somalia, Sudan, na Yemen.
Trump alichukua uamuzi huu kufuatia shambulio lililotokea hivi karibuni katika jimbo la Colorado ambapo watu 15 waliuawa.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani (White House) imesema kuwa raia wa nchi nyingine saba pia wamezuiwa kuingia Marekani kwa sababu “wanaleta hatari kubwa” kwa nchi hiyo.
Nchi hizo ni Burundi, Cuba, Laos, Sierra Leone, Togo, Turkmenistan, na Venezuela.
Marufuku hiyo kwa raia wa nchi hizo inakuja wakati ambapo serikali ya Trump inaendeleza mpango wa kuwafukuza wahamiaji mamilioni kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Hii inajumuisha takriban watu 37,000 ambao taarifa zinasema Trump aliwafukuza katika mwezi wa kwanza wa utawala wake.
Kwa sasa, taarifa zinaonyesha kuwa Washington iko kwenye mazungumzo na nchi kama Rwanda ili zipokee wahamiaji watakaofukuzwa.




