Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa Israel imekubali “masharti muhimu” ya kusitisha mapigano kwa siku 60 huko Gaza.
Kupitia ujumbe alioweka kwenye jukwaa lake la mitandao ya kijamii la Truth Social, Trump alisema kuwa wakati wa kipindi hicho cha usitishaji vita, Marekani itashirikiana na pande zote ili kumaliza vita hivyo.
Trump aliandika:
“Waqatar na Wamisri wamefanya kazi kubwa kusaidia kuleta Amani. Watawasilisha pendekezo la mwisho. Ninaamini… Hamas watakubali makubaliano haya…”
Israel haijathibitisha rasmi iwapo imekubali masharti hayo, na Hamas haijatoa taarifa yoyote kufikia sasa.
Tangazo hili la Trump limekuja kabla ya mkutano wake wiki ijayo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambapo alisema atazungumza kwa msimamo mkali.
Siku ya Jumanne, tarehe 1 Julai 2025, Trump pia alisema kuwa anaamini kuwa Netanyahu anataka kumaliza mapigano huko Gaza.
Israel ilianzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Gaza baada ya shambulio la Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa. Wizara ya Afya ya Palestina inayoendeshwa na Hamas imesema kuwa angalau watu 56,647 wameuawa huko Gaza tangu wakati huo.




