Jeshi la Urusi lilizindua mashambulizi ya usiku kwa kutumia ndege zisizo na rubani (drones) na makombora dhidi ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, usiku wa kuamkia Julai 4, 2025, yakilenga maeneo mbalimbali, ikiwemo maeneo ya raia.
Kwa mujibu wa Tymur Tkachenko, kiongozi wa utawala wa kijeshi wa Kyiv, watu wanane walijeruhiwa katika mashambulizi hayo yaliyodumu kwa saa nyingi na kusababisha uharibifu wa majengo marefu katika maeneo mawili ya jiji.
Mashambulizi haya yalifanyika saa chache tu baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutangaza kuwa mazungumzo yake ya simu na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, hayakufanikisha lolote kuhusu kusitisha vita.
Trump alisema:
“Tulizungumza kwa muda mrefu. Tulijadili mambo mengi, yakiwemo vita vya Ukraine, lakini hakuna kilichotokea.”
Wakati huo huo, mashambulizi ya Urusi yamezidi kuongezeka. Ukraine inadai kuwa katika mwezi wa Juni pekee, ilishambuliwa kwa zaidi ya makombora 330 na drones 5,000.
Kwa sasa, serikali ya Trump imeamua kusitisha baadhi ya misaada ya kijeshi kwa Ukraine — ikiwa ni pamoja na makombora ya ulinzi wa anga — kwa sababu ya kutaka kulinda akiba ya silaha za Marekani.
Ingawa Trump hakumkabili moja kwa moja Putin, vyombo vya habari vya serikali ya Urusi (TASS) vinaripoti kuwa Trump alieleza kuwa angependa vita hiyo imalizike haraka, lakini Putin alimjibu kuwa Urusi “haitarudi nyuma” katika malengo yake ya kivita.



