Muungano wa Alliance Fleuve Congo (AFC), unaojumuisha waasi wa M23, umetangaza kuwa makubaliano ya amani yaliyosainiwa hivi karibuni kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ni hatua muhimu lakini isiyotosha.
Taarifa hiyo ilitolewa na mratibu wa muungano huo, Corneille Nangaa, kupitia hotuba aliyotoa kwa wananchi wa Congo katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa DRC.
Mnamo Ijumaa, tarehe 27 Juni, Rwanda na DRC walisaini makubaliano ya amani katika sherehe iliyofanyika Washington DC, Marekani.
Makubaliano hayo yalikuja baada ya miaka mitatu ya uhusiano mgumu kati ya mataifa hayo mawili, kutokana na vita vya serikali ya Kinshasa dhidi ya waasi wa M23, kundi ambalo jamii ya kimataifa inadai linaungwa mkono na Rwanda.
Mojawapo ya vipengele vya makubaliano hayo ni kwamba mgogoro kati ya M23 na serikali ya DRC utashughulikiwa kupitia mazungumzo ya Doha nchini Qatar.
Katika hotuba yake, Nangaa alikosoa makubaliano hayo kwa kushughulikia upande mmoja tu wa tatizo na kupuuza mizizi halisi ya mzozo wa Congo.
Alisema:
“Kudanganya wananchi na dunia kuwa hakuna tatizo la ndani nchini DRC, kwamba ni suala tu kati ya Kigali na Kinshasa, ni ulaghai usiovumilika.”
Aliongeza kuwa ndiyo maana AFC/M23 inaunga mkono mazungumzo ya Doha, yenye lengo la kuanzisha majadiliano ya kweli kati ya Kinshasa na harakati yao, ili kutatua sababu halisi za mgogoro wa Congo.
Pia alisifu juhudi, uvumilivu, na nia njema ya Qatar na Emir wake, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, katika kutafuta amani ya kudumu.
Nangaa alihitimisha kwa kusema kwamba madai ya AFC/M23 hayajabadilika, na kwamba amani ya kweli itapatikana tu pale Wacongo watakapohusishwa moja kwa moja katika kutafuta suluhisho la kiini cha mgogoro, ambao aliutupia lawama kwa utawala wa Rais Tshisekedi.




