Askofu Dr. Emmanuel Musinga, mhubiri anayeishi Marekani, ameyataka mataifa ya Afrika yaige mfano wa Rwanda, kutokana na usalama, huduma bora na mfumo mzuri wa utawala nchini humo, akisema kuwa Rwanda imepiga hatua nje ya kiwango cha Afrika.
Askofu huyo ambaye asili yake ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, aliyasema haya katika mahojiano na One Nation Radio, akieleza kuwa analifahamu Rwanda zaidi kuliko anavyoijua Kongo, kwa sababu hulitembelea kila mwaka.
Alisema:
“Ninalijua Rwanda zaidi ya DRC kwa sababu nimeishi Rwanda kwa muda mrefu kuliko nilivyoishi Kongo.”
Pia alieleza kuwa ndugu zake wengi wa Banyamulenge walipitia Rwanda kabla ya kuhamia Marekani.
Alipoulizwa kuhusu mtazamo wake kwa Rwanda, alisema ni nchi inayotoa huduma bora za umma, kama zile za Marekani na mataifa makubwa ya Ulaya.
Aliongeza:
“Rwanda ina huduma bora, zinazofanana na za Marekani na nchi kubwa za Ulaya. Sasa siyo tena ya kiwango cha Afrika.”
Alieleza kwamba pasipoti ya Rwanda hutolewa ndani ya siku tatu, na kwamba huduma nyingi zinapatikana kwa njia za kidigitali.
Alitumia nafasi hiyo kuyahimiza mataifa mengine ya Afrika kujifunza kutoka Rwanda, kuhusu jinsi ya kuboresha huduma. Anasema kama Afrika ingezingatia mfano wa Rwanda, basi bara hilo lingeweza kuwa kielelezo cha kimataifa cha huduma bora.
Askofu Musinga pia alimsifu Rais wa Rwanda, Paul Kagame, akisema anachokipenda ni kwamba anawapenda wananchi wake na nchi yake.
Alisema Kagame ni mtu mwenye hekima, na anayekubali kila wazo au hatua inayoleta maendeleo kwa watu wake na taifa lake.
Akihitimisha mahojiano hayo, Dr. Musinga alisema Kagame ni mzazi kwa watu wote wenye fikra chanya, na kwamba kumfuatilia kwa karibu kunaweza kuboresha maisha yako kwa kiwango kikubwa.
Kabla ya kuhamia Marekani, Dr. Musinga aliishi Kenya, baada ya kutoka Rwanda alikoingia kwa mara ya kwanza mwaka 1994.
Kwa sasa, Askofu Dr. Emmanuel Musinga anaongoza makanisa nchini Marekani, Kenya, Uganda, na maeneo mengine.




