Barnabé Kikaya Bin Karubi, mshauri wa karibu wa Joseph Kabila Kabange na rafiki yake wa muda mrefu, amekanusha madai kuwa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo anaunga mkono Rwanda.
Madai haya yanatolewa na serikali ya Rais Félix Antoine Tshisekedi, aliyemrithi Kabila madarakani.
Shutuma kwamba Kabila anaunga mkono Rwanda na waasi wa M23 ziliongezeka mwezi Aprili mwaka huu, baada ya Kabila kutangaza kuwa anarejea kutoka uhamishoni kwenda mjini Goma, ambao umekuwa chini ya udhibiti wa M23 kwa takribani miezi mitano.
Karubi, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mawasiliano, Katibu binafsi wa Kabila na mshauri wake wa kidiplomasia, aliiambia ACTUALITE.CD kwamba shutuma hizo ni za uongo na zinalenga kumharibia sifa Kabila kwa wananchi.
Alisema:
“Sidhani kama Rais Kabila anaunga mkono Rwanda. Rwanda ni jirani yetu, na itabaki hivyo milele. Hili halipaswi hata kuulizwa, kwa sababu Rais Kabila hana mamlaka ya kupinga taifa jirani.”
Aliendelea:
“Rais Kabila yuko Goma, mji unaodhibitiwa na waasi wa M23. Kauli kwamba anaungwa mkono na Rwanda ilishika kasi hata katika vyombo vya habari vya Magharibi, lakini sasa wanajiondoa kwenye hiyo hoja.”
Karubi alikiri kuwa M23 ni kikundi chenye nguvu kijeshi, kilichoonyesha uwezo wake wakati wa mapambano ya kuchukua Goma, ambapo kiliwashinda wanajeshi kutoka nchi za SADC na mamluki wa kizungu.
Alisema yeye na Kabila wana lengo moja — kumaliza utawala wa kidikteta wa Rais Félix Tshisekedi.
Alisema:
“Waasi walioko Goma wanapambana na udikteta. Ndipo maslahi yetu yanapokutana — sisi pia, pamoja na wapinzani wasio na silaha wanaomuunga mkono Rais Kabila, tumeamua kuutokomeza udikteta. Hicho ndicho watu wa Congo wanakitarajia. Tunapaswa kuwakomboa — na tutafanikiwa.”
Karubi aliongeza kuwa Kabila yuko Goma kwa sababu ni mahali pekee anapojisikia salama, baada ya mateso ya muda mrefu kutoka kwa serikali ya Kinshasa, ambayo ilimnyang’anya kinga yake ya kisheria na kutishia kumpeleka mahakamani.
Alisisitiza kuwa kuwa kwake Goma haipaswi kuchukuliwa kama tatizo, kwani licha ya kuwa chini ya M23, Goma bado ni sehemu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.




