Nchini Burundi, zaidi ya dola milioni 15 za Kimarekani zilizotarajiwa kuingia kwenye hazina ya serikali kwa mwaka wa fedha 2023–2024 zimepotea bila maelezo, kwa mujibu wa Waziri wa Fedha, Ntahontuye Nestor.
Mtaalamu wa uchumi na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Massachusetts, Léonce Ndikumana, alisema kuwa kati ya mwaka 2000 na 2019, Burundi iliripoti kuuza dhahabu yenye thamani ya dola milioni 765, ilhali nchi zilizonunua zinasema zililipa dola bilioni 1.4. Hii inaacha pengo la dola milioni 635 ambazo hazijaelezwa zilienda wapi.
Katika juhudi za kutatua tatizo hili, serikali ya Burundi ilisitisha mikataba na makampuni ya uchimbaji madini mwaka 2023, kwa lengo la kusimamia sekta ya madini kwa uhuru.
Mmoja wa wapiganaji wa zamani, Marcel Nduwayo, alimwambia Rais Évariste Ndayishimiye kuwa nchi inakabiliwa na wizi mkubwa. Alitoa mfano wa Rwanda ambapo sampuli za madini hupimwa haraka, lakini Burundi huchukua saa nyingi na mara nyingine hutolewa visingizio visivyoeleweka. Alisema: “Kama si kugawana mali, basi ni hila na hofu.”
Katika kikao na viongozi wa ngazi za chini mnamo Machi 2025, Rais Ndayishimiye alisema kuwa ukosefu wa bidhaa za petroli unasababishwa na uporaji unaofanywa na baadhi ya viongozi. Alisema: “Sielevi ni kwa nini nchi yenye madini mengi kama yetu bado ni maskini. Katika mkoa wa Cibitoke tulikuta dhahabu yenye usafi wa 87%. Sielewi ni kwa nini hatuendelei.”
Rais aliahidi zawadi ya asilimia 10 kwa mwananchi yeyote atakayetoa taarifa kuhusu madini yaliyofichwa na viongozi wa serikali.




