Wakati bei ya dhahabu ilipoongezeka kwa kasi mwaka 2025, athari zake zilionekana sana katika eneo la Sahel, Afrika Magharibi, linalokumbwa na vita, vurugu, na ukosefu wa usalama.
Nchi za Burkina Faso, Mali, na Niger zina utajiri mkubwa wa dhahabu, inayochimbwa hasa kupitia uchimbaji haramu na usiofuatiliwa rasmi, maarufu kama uchimbaji wa wananchi. Ingawa uchimbaji huu huingiza mabilioni ya dola, fedha hizo hazifiki kwa raia wa kawaida.
Serikali za kijeshi zinazotawala nchi hizo zinajaribu kunufaika na dhahabu hiyo kufadhili vita dhidi ya makundi ya kigaidi kama al-Qaeda na Islamic State, na pia kuimarisha utawala wao unaoungwa mkono na Urusi.
Kikundi cha mamluki cha Wagner, na sasa Africa Corps, kinashirikiana na serikali hizo. Kinadaiwa kulipwa kwa dhahabu au kupewa haki za kuchimba madini, huku pia kikihusishwa na ukandamizaji mkubwa wa haki za binadamu.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), mapato kutoka kwa dhahabu haramu yanaendelea kufadhili ugaidi, ikiwemo JNIM (Jama’at Nusrat al-Islam wal-Muslimin), hali inayosababisha mapigano makali zaidi.
Ingawa dhahabu hiyo huuza katika masoko ya kimataifa, hasa Falme za Kiarabu (UAE), ni vigumu kufuatilia asili yake, jambo linalowezesha dhahabu ya damu kuingia sokoni bila vizuizi.
Wataalam wanasema hii ndiyo “dhahabu mpya ya damu” barani Afrika, lakini hakuna sheria za kimataifa za kuizuia kama zile zilizowekwa kwa almasi za vita.
Wakati nchi maskini za Sahel zinapambana kulinda usalama na uhuru wao, dhahabu ambayo ingekuwa chanzo cha maendeleo, sasa imekuwa chanzo cha maangamizi na huzuni.




