Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imeanza juhudi za kuzuia Rwanda kuchukua uongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Kati (CEEAC).
Jumamosi tarehe 7 Juni, mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa CEEAC ulianza mjini Malabo, Guinea ya Ikweta.
Mkutano huo unahudhuriwa na wawakilishi kutoka Angola, Congo-Brazzaville, DRC, Cameroon, Gabon, Chad, Guinea ya Ikweta, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Rwanda, Burundi, na São Tomé & Príncipe.
Ajenda kuu ya mkutano huo ni kukabidhiana uongozi kutoka kwa Guinea ya Ikweta hadi kwa Rwanda, ambayo ndiyo inayofuata kuongoza jumuiya hiyo.
Hata hivyo, Jeune Afrique imeripoti kuwa Kinshasa inapinga vikali Rwanda kuongoza CEEAC kutokana na mvutano wa kisiasa uliopo kati ya mataifa hayo mawili.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, siku ya Alhamisi, wakati wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje uliofanyika Malabo, Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda wa Guinea ya Ikweta, Lucas Abaga Nchama, aliwaleta pamoja wawakilishi wa Rwanda na DRC kujadili hali ya uhasama iliyodumu kwa muda.
Kutokana na migogoro hiyo ya kidiplomasia, DRC inadaiwa kujaribu kuzuia Rwanda kuchukua uongozi, hadi Rwanda kutishia kujiondoa kwenye jumuiya hiyo iwapo itakataliwa.
Kinshasa nayo imesema kuwa ikitokea Rwanda ikaongoza CEEAC, basi nao wanaweza kufikiria kujiondoa.
Si mara ya kwanza Rwanda na DRC kutofautiana ndani ya CEEAC.
Jeune Afrique inakumbusha kuwa miaka miwili iliyopita, Rais Paul Kagame aliandika barua kwa Rais wa Comoros, Azali Assoumani, aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika wakati huo, akieleza kutoridhika kwa Rwanda kwa kuzuiwa kushiriki katika Mkutano wa 22 wa kawaida wa CEEAC uliofanyika tarehe 25 Februari 2023 mjini Kinshasa.
Uamuzi huo ulitokana na agizo la Rais Félix Tshisekedi aliyekuwa akiongoza CEEAC wakati huo.




