Gavana wa jimbo la Haut-Katanga, Jacques Kyabula, ameitwa kuja Kinshasa kutoa maelezo kuhusu kauli alizotoa kuhusu Rais wa zamani Joseph Kabila Kabange na Corneille Nangaa, kiongozi wa muungano wa AFC/M23.
Wito huo ulitolewa na Waziri wa Usalama wa Ndani, Jacquemin Shabani, ingawa taarifa zinaeleza kwamba uliamriwa moja kwa moja na Rais Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo.
Katika barua rasmi aliyoandikiwa, Kyabula aliamriwa “kusitisha shughuli zote na kufika Kinshasa ndani ya saa 48.”
Kyabula aliitwa muda mfupi baada ya kusema hadharani kwamba “chanzo halisi cha vita mashariki mwa DRC ni Kagame, siyo Kabila wala Nangaa.”
Akaongeza: “Kabila na Nangaa ni Wacongo, matatizo yao yanapaswa kutatuliwa kifamilia.”
Kauli hizi zinakinzana na msimamo wa serikali ya Kinshasa, inayowachukulia Kabila na Nangaa kama wasaliti na maadui wakuu wa taifa.
Corneille Nangaa tayari amehukumiwa kifungo cha maisha jela, baada ya kuungana na waasi wa M23 na kuanzisha muungano wa Alliance Fleuve Congo, unaolenga kumwondoa madarakani Rais Tshisekedi.
Tangu Kabila alipotembelea mji wa Goma unaoshikiliwa na M23, serikali ya Kinshasa inamshutumu pia kwa kuunga mkono uasi huo.




