Jumamosi hii, waasi wa M23 walifanya msako mkali mjini Goma, hasa katika eneo la Ndosho, Wilaya ya Karisimbi, na kuwakamata takriban watu 30, wakiwemo wapiganaji wa FDLR, pamoja na bunduki 10 na magazini zake.
Meya wa Jiji la Goma, Katembo Ndalieni Julien, aliipongeza operesheni hiyo na kuwaomba wakazi watoe taarifa kuhusu watu wanaohatarisha usalama, akisema:
“Bunduki kama hii inaweza kufichwa ndani ya koti, mtu akatoka usiku na kuleta vurugu. Tujulishe, nasi tutawaletea amani.”
Meya huyo pia aliwasihi wale ambao wana ndugu katika kundi la Wazalendo wawashauri waweke silaha chini, na kukemea tabia ya watu kujihukumia wenyewe, badala ya kuacha mahakama ifanye kazi yake.
Tangu M23 walipouteka mji wa Goma mwishoni mwa Januari 2025, kumeongezeka kwa matukio ya uhalifu wa kutumia silaha, hasa baada ya wanajeshi wa serikali kushindwa na kuacha silaha ambazo zilisambaa kwa raia.
Msemaji wa kijeshi wa M23, Luteni Kanali Willy Ngoma, alithibitisha kuwepo kwa wapiganaji wa FDLR miongoni mwa waliokamatwa, na akaishutumu serikali ya DRC kwa kufadhili machafuko mjini Goma na Bukavu kupitia baadhi ya wanasiasa wake.




