India imetangaza rasmi kwamba imeshambulia maeneo tisa yanayodhibitiwa na Pakistan kwa makombora, katika oparesheni waliyoipa jina la “Operation Sindoor”, shambulio ambalo linadaiwa kusababisha vifo vya watu kadhaa.
Kwa upande wake, Pakistan imesema ilijibu mashambulizi hayo kwa kushambulia ngome na miundombinu ya kijeshi ya India, na kudai kuangusha ndege tano za kivita za India pamoja na kuwakamata wanajeshi wa India kama mateka wa vita.
Mashambulizi ya usiku huo kutoka India yamefanyika katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Pakistan na pia katika jimbo la Punjab, upande wa mashariki mwa Pakistan. Miji ya Muzaffarabad na Kotli, yote katika Kashmir, ndiyo iliyolengwa zaidi.
Hadi sasa, Pakistan imethibitisha kuwa watu wanane wamefariki dunia kufuatia mashambulizi hayo na wengine takribani 35 kujeruhiwa.
Waziri wa Ulinzi wa Pakistan, Khawaja Asif, ametangaza kuwa majeshi ya nchi hiyo katika kujibu mashambulizi hayo yameangusha ndege tano za kijeshi za India na kuwakamata wanajeshi wa India kama mateka.
Akaongeza kwa kusema:
“Pakistan italipiza kisasi dhidi ya shambulio lolote kutoka India, na kwa sasa, tunaendelea kujibu mashambulizi haya ya India.”
Pakistan imesema kuwa India ilivurumisha makombora katika maeneo matano ndani ya mipaka yake.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Uingereza, Reuters, mara baada ya India kushambulia, majeshi ya nchi hizo mbili yalibadilishana makombora na risasi nzito, huku milio mikubwa ya silaha ikisikika katika maeneo matatu ya mipakani mwa mataifa hayo.
Baada ya kuibuka kwa mapigano haya, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amezitaka pande zote mbili kuchukua hatua za haraka za kusitisha mapigano na kuanzisha mazungumzo ya amani ili kuepusha hali kuzidi kuwa mbaya.
Tukio hili la kijeshi linakuja katika kipindi ambacho uhusiano kati ya India na Pakistan umedorora sana, hasa baada ya watalii 26 kuuawa katika eneo la Kashmir upande wa India.
India ilimtupia lawama Pakistan kwa shambulio hilo lililotokea mwezi uliopita, madai ambayo Pakistan imeyakataa vikali.




