240923-Abbas-Araghchi-mb-1226-d1ad0c

Iran Yapinga Vikali Mashambulizi ya Marekani Dhidi ya Vituo Vyake vya Nyuklia

Iran imepinga vikali mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Marekani siku ya Jumapili, ambapo vituo vitatu vikuu vya utafiti wa nyuklia vilivyoko Fordo, Isfahan, na Natanz vililengwa.

Serikali ya Iran imetangaza kuwa mashambulizi hayo ni kitendo cha uchokozi wa hali ya juu, ikisema kuwa Marekani imevuka “mstari mwekundu,” yaani mipaka ya uvumilivu wa Iran.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya Iran, mashambulizi hayo yalifanywa na ndege za kivita za Marekani na yalisababisha uharibifu wa miundombinu, lakini hayakusitisha kabisa shughuli za kawaida katika vituo hivyo.

Iran inasema kuwa mashambulizi hayo yalilenga kurudisha nyuma maendeleo yake ya kisayansi katika nyanja ya nyuklia, lakini imesisitiza kuwa hayatavuruga mpango wake wa nyuklia wa “amani.”

Hayo yalisemwa na Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Amir Saeid Iravani, wakati wa kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambapo alisisitiza kuwa Marekani imechagua njia ya vita badala ya mazungumzo, na Iran haitakaa kimya.

Balozi Iravani alisema kuwa jeshi la Iran linaandaa namna, mkakati na kiwango cha majibu yanayofaa kwa mashambulizi hayo, ingawa hakutaja muda wala mbinu zitakazotumika kulipiza kisasi, lakini akasisitiza kuwa serikali na jeshi vinaendelea na maandalizi kwa kina.

Iran imechukulia mashambulizi hayo kama ukiukwaji wa mamlaka ya taifa lake. Maafisa wa kijeshi na wa masuala ya kigeni walifanya mikutano ya dharura ili kupanga hatua zitakazochukuliwa endapo Iran itaamua kulipiza kisasi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alielekea haraka Moscow kwa mazungumzo na Urusi, mshirika wake wa karibu, kujadili hatua zitakazofuata baada ya mashambulizi hayo.

Wakati mapigano kati ya Iran na Israel yakizidi kuwa makali, dunia ina wasiwasi mkubwa kuwa huenda hali hiyo ikasababisha vita kubwa ya kikanda ambayo itabadilisha hali ya usalama duniani na kanuni kuhusu matumizi ya silaha za nyuklia.

Wataalamu wa kimataifa wanaonya kuwa mashambulizi haya ya kijeshi yanaweza kuathiri juhudi za amani za kuzuia ueneaji wa silaha za nyuklia, huku Iran ikishutumiwa kwa muda mrefu na baadhi ya nchi kuwa inaendelea kisiri na mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia – madai ambayo Iran inakanusha.

Tehran sasa inasema haina njia nyingine ila kujilinda na kulipiza kisasi, hali inayozidisha wasiwasi wa vita katika eneo lote, huku dunia ikingoja kuona kama bado kuna nafasi ya kurudi kwenye meza ya mazungumzo au kama vita vya wazi haviepukiki tena.

Sangiza iyi nkuru

Soma Izindi Nkuru

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *