Mossad – Idara ya Kijasusi ya Israel
Mossad, neno la Kiebrania linalomaanisha “Taasisi”, ni shirika la kijasusi la Israel linaloshughulikia ujasusi wa nje, operesheni za siri, na vita dhidi ya ugaidi. Inafanya kazi pamoja na Aman (jasusi wa kijeshi) na Shin Bet (usalama wa ndani). Ni Waziri Mkuu wa Israel pekee ndiye anayeidhinisha operesheni zake kubwa.
Kwa mujibu wa Wikipedia, Mossad ina bajeti ya kila mwaka ya takriban shekeli bilioni 10 za Israel (sawa na dola bilioni 2.73 za Marekani) na inaajiri watu takribani 7,000.
Mossad inahesabiwa kuwa miongoni mwa mashirika ya kijasusi yenye nguvu zaidi duniani.
Katika mfululizo huu wa makala, tunatazama baadhi ya operesheni zilizothibitishwa rasmi na Israel, kama vile kumkamata Otto Adolf Eichmann, mmoja wa viongozi wa Kinazi waliohusika moja kwa moja na mauaji ya Wayahudi (Holocaust).
Lakini katika makala hii, tunakuonesha jinsi Mossad ilivyofanikiwa kuingilia njia za mawasiliano za Hezbollah – kundi la Kishia kutoka Lebanon linaloonekana kama tishio kwa Israel na ambalo limetangazwa kuwa la kigaidi na nchi mbalimbali.
Shambulio la Septemba 17, 2024 mjini Beirut
Mnamo Septemba 17, 2024, majira ya saa tisa alasiri (15:00), katika soko la mjini Beirut – mji mkuu wa Lebanon – kamera za usalama zilinasa tukio lisilo la kawaida. Mwanaume aliyekuwa amepokea ujumbe wa siri kupitia redio ya mawasiliano (talkie-walkie) alilipuliwa ghafla baada ya kufungua ujumbe huo.
Kamera zilionyesha wazi jinsi kifaa kilivyolipuka mikononi mwake mara tu baada ya ujumbe kupokelewa. Tukio hili lilishtua raia wa Lebanon.
Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, ujumbe huo ulitoka kwa makamanda wakuu wa Hezbollah.
Gazeti la Israel, The Jerusalem Post, katika toleo lake la Septemba 18, 2024, lilithibitisha kuwa Mojtaba Amani, balozi wa Iran nchini Lebanon, alikuwa miongoni mwa waliojeruhiwa kutokana na milipuko hiyo.
Maelezo ya kina ya tukio
Video zilizosambaa ziliwaonesha watu waliokuwa wakipokea ujumbe kupitia redio hizo, kisha kifaa hicho kililipuka kwa nguvu. Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 2,800 walijeruhiwa katika maeneo tofauti ya Lebanon kutokana na redio hizo.
Redio hizi za mawasiliano ni za zamani (kutoka miaka ya 1980), lakini bado hutumika na majeshi au mashirika ya usalama kutokana na usalama wake na ugumu wa kudukuliwa.
Hezbollah, chini ya uongozi wa zamani wa Hassan Nasrallah, ilikuwa imepiga marufuku matumizi ya simu kwa wanachama wake ili kuepuka ujasusi. Badala yake, walitegemea redio hizi – lakini kumbe Mossad ilikuwa tayari imechukua hatua.
Nasrallah mwenyewe aliuawa mjini Beirut kwa shambulio la angani lililofanywa na Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF).
Hofu na taharuki yaikumba Lebanon
Baada ya mlipuko wa kwanza, mingine ilifuata kote nchini. Wanachama wa Hezbollah na raia wengine walianza kutupa redio zao kwa hofu. Katika mazishi ya baadhi ya wahanga yaliyoandaliwa siku iliyofuata, mlipuko mwingine uliua watu 37, kujeruhi wengine 3,700, na kuacha maelfu wakiwa na mshtuko wa kiakili.
Hospitali za Beirut zilijaa watu waliojeruhiwa usoni, mikononi, na sehemu za siri kutokana na milipuko ya karibu.
Ni mbinu gani Mossad ilitumia?
Wachunguzi walikuja na maelezo mawili ya uwezekano wa mbinu zilizotumika:
Shambulio la kidijitali (cyberattack): Inaaminika kuwa Mossad ilituma amri kupitia mtandao ambayo ilisababisha betri ya kifaa kupasha joto hadi kulipuka. Lakini wataalamu wengi walipinga hili kwa kusema kwamba joto pekee haliwezi kusababisha mlipuko mkubwa kiasi hicho.
Kifaa kilichoandaliwa kwa vilipuzi: Inawezekana Mossad ilipachika vilipuzi vidogo ndani ya redio hizo wakati wa uzalishaji. Chipu ndogo iliyowekwa ndani yake iliweza kuamriwa kuwasha betri, ambayo kisha ililipuka ghafla.
Baadhi ya video zinaonesha magari karibu na wahanga yakiteketea baada ya milipuko hiyo, jambo linalodhihirisha nguvu ya vilipuzi vilivyotumika.
Asili ya vifaa hivyo
Uchunguzi ulionyesha kuwa redio hizo zilidaiwa kutengenezwa na kiwanda kiitwacho Gold Apollo kutoka Taiwan. Hata hivyo, mkurugenzi wake alikana kuhusika, akisema walikodisha kazi hiyo kwa kampuni nyingine: BA.C Consulting.
Kampuni hiyo iliripotiwa kuwa na makao yake Budapest, Hungary, lakini mamlaka za Hungary zilikanusha kuwa kampuni hiyo ipo au imewahi kutengeneza vifaa vya mawasiliano.
Gazeti la New York Times, likinukuu maafisa wa kijasusi, lilidai kuwa kampuni hiyo ilikuwa na uhusiano wa moja kwa moja na Mossad.
Pia, baadhi ya vipande vilivyopatikana vilikuwa na alama ya ICOM, kampuni ya Kijapani ambayo ilisitisha utengenezaji wa vifaa hivyo tangu mwaka 2014.
Wataalamu wanasema ni vigumu sana kufuatilia chanzo halisi cha vifaa hivyo, kwa kuwa kuna viwanda vya kughushi bidhaa katika maeneo kama China.
Operesheni ya hali ya juu
Mtaalamu mmoja aliyefanya mahojiano na gazeti la L’Orient-Le Jour alisema kuwa operesheni hii ilikuwa ya kiwango cha juu na iliyopangwa kwa uangalifu mkubwa na Mossad. Pia alisema ilileta pigo kubwa la kiakili kwa Hezbollah.
Hata hivyo, alionya kuwa operesheni hiyo ilisababisha hofu kubwa kwa raia wa kawaida wa Lebanon. Watu wengi waliepuka mikusanyiko na walihofia kutumia vifaa vya kielektroniki kwa kuogopa kulipuliwa.




