Serikali ya Kenya imetangaza kuanzisha uchunguzi maalum dhidi ya watu kutoka Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na jamii ya Wagisu kutoka Uganda wanaoishi katika kaunti ya West Pokot.
Hatua hii imechukuliwa baada ya watu 13 kukamatwa katika eneo la Bendera, wakituhumiwa kwa makosa ya kula nyama ya binadamu na biashara haramu ya viungo vya miili ya watu.
Kamishna wa Kaunti ya West Pokot, Khalif Abdullahi, alisema baadhi ya washukiwa tayari wamekiri makosa, na walikuwa wanaishi kinyume cha sheria kwenye ardhi iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Alisema makazi hayo yatabomolewa, na watu hao watapitiwa uchunguzi wa kina.
Maafisa wa Kenya walisema kuwa ingawa kuna ushirikiano wa kieneo kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hilo haliondoi jukumu la taifa kulinda usalama wa ndani, hivyo ukaguzi huu wa wakazi wa kigeni utaendelea kufanyika.
Uchunguzi bado unaendelea, huku washukiwa hao 13 wakizuiliwa kwa siku 21 ili kuruhusu mwendesha mashtaka kukusanya ushahidi.




