Katika Mkutano wa Kimataifa wa Usalama wa Afrika (ISCA) uliofanyika Kigali, Rwanda ilizindua rasmi silaha za kisasa zinazotengenezwa ndani ya nchi na kampuni ya REMCO (Rwanda Engineering and Manufacturing Corporation), ambayo imekuwa ikitengeneza vifaa vya kijeshi kwa Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF).
Silaha zilizozinduliwa ni pamoja na bastola ndogo na kubwa, bunduki za masnipa, silaha za ardhini, na zile zinazotumika katika vita dhidi ya ugaidi. REMCO iko katika Wilaya ya Gasabo, kwenye eneo la viwanda ambalo sasa ni kitovu cha uwezo wa Rwanda katika utengenezaji wa vifaa vya kijeshi.
Miongoni mwa silaha zilizowasilishwa ni bastola, bunduki kama ARAD5/300BKL inayofikia umbali wa mita 500, na bunduki za masnipa kama ACE SNIPER na ARAD SNIPER zenye uwezo wa kufyatua risasi hadi mita 800. Pia kulikuwa na bunduki kubwa aina ya Machine Gun kama NEGEV ULMG, na vifaa vya kuona usiku (night vision).
Ingawa baadhi ya vipande vya silaha kama risasi, magazini, na lenzi bado huagizwa kutoka nje, sehemu kubwa ya vifaa hutengenezwa ndani ya nchi. Hii inaonyesha hatua kubwa ambayo Rwanda imepiga katika kujitegemea kwa masuala ya usalama.
Wizara ya Ulinzi imethibitisha kuwa silaha hizi zimeidhinishwa kwa matumizi ya kijeshi na tayari zinatumika na RDF pamoja na majeshi rafiki kutoka nchi nyingine. REMCO inashirikiana na kampuni ya Israel ya IWI (Israel Weapon Industries), inayotoa maarifa na teknolojia ya kusaidia katika uzalishaji wa silaha hizo.
Mkutano wa ISCA ulihudhuriwa na nchi mbalimbali za Afrika na washirika wa kijeshi wa Rwanda, ambapo pia walionyesha vifaa vyao vya kijeshi kutoka Misri, Uturuki na kwingineko. Rwanda kutengeneza silaha zake ni hatua muhimu kuelekea kujitegemea na kujenga uwezo wa usalama wa muda mrefu.





