Bodi ya Maendeleo ya Rwanda (RDB) imetangaza kuwa sherehe ya Kwita Izina, hafla ya kipekee ya kuwapa majina watoto wa sokwe wa milimani, itafanyika tarehe 5 Septemba 2025, baada ya kuahirishwa awali kutokana na mlipuko wa virusi vya Marburg.
Kawaida, tukio hili linafanyika katika eneo la Kinigi, Wilaya ya Musanze, karibu na makao makuu ya Hifadhi ya Taifa ya Volcanoes, na huhudhuriwa na watu mashuhuri, raia wa Rwanda, na wageni kutoka nje ya nchi wanaokuja kushuhudia tukio hili la kipekee la uhifadhi wa mazingira.
Sherehe ya mwaka huu ni toleo la 20 tangu ianzishwe. Awali ilipangwa kufanyika Oktoba 18, 2024, ambapo watoto 22 wa sokwe waliozaliwa tangu Septemba 2023 walitakiwa kupewa majina, lakini tukio hilo liliahirishwa bila sababu rasmi kutajwa na RDB.
Sasa RDB imethibitisha kuwa hafla hiyo itafanyika Septemba 5, 2025.
Kwita Izina ilianzishwa rasmi na serikali ya Rwanda mnamo mwaka 2005 kama sehemu ya kudumu ya kuhifadhi sokwe, kutambua mchango wa wale wanaowatunza kila siku, na kusherehekea mafanikio ya uhifadhi kwa jamii zinazozunguka hifadhi.
Hadi sasa, sokwe 352 wamepewa majina katika kipindi cha miaka 19 iliyopita.
Katika toleo la mwaka 2023 (la 19), RDB ilitangaza kuwa toleo la 20 litakuwa maalum, kwani watu wote waliowahi kushiriki kama waweza-majina miaka iliyopita watakaribishwa.
Ripoti ya mwaka 2024 ya RDB kuhusu uwekezaji, utalii, mauzo ya nje, na biashara, inaonyesha kuwa utalii uliingizia Rwanda dola milioni 647 za Kimarekani, ikiwa ni ongezeko la 4.3% ikilinganishwa na mwaka uliotangulia. Utalii wa sokwe ulichangia asilimia 27 ya mapato hayo.




