Kundi la waasi la M23, linalopinga serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), limewarejesha rasmi wajumbe wake waliokuwa wakihudhuria mazungumzo ya amani huko Doha, Qatar, na serikali ya Kongo.
Wawakilishi hao wa M23, waliokuwa kwenye mazungumzo hayo kwa muda wa siku 30, sasa wameitwa kurudi Goma.
Mwandishi huru Steve Wembi, ambaye kwa sasa ana uhusiano wa karibu na M23 pamoja na muungano wa Alliance Fleuve Congo (AFC) ambao M23 ni sehemu yake, ametangaza kwamba wajumbe hao wakiongozwa na Benjamin Mbonimpa (katibu mkuu wa kudumu wa AFC/M23), walirudi mwanzoni mwa wiki hii.
Hadi sasa, Kinshasa wala M23 hawajatoa taarifa kamili kuhusu walichokubaliana katika mazungumzo hayo.
Mnamo Aprili mwaka huu, pande zote mbili zilitoa taarifa ya pamoja zikisema zimekubaliana juu ya kusitisha mapigano ili kutoa mazingira mazuri ya mazungumzo ya amani.
Mazungumzo hayo, kulingana na Kinshasa na M23, yalilenga “mizizi ya mzozo unaoendelea na suluhisho la kudumu la kuumaliza mashariki mwa DRC.”
Wawakilishi wa DRC na AFC/M23 walikubaliana kutekeleza makubaliano hayo hadi mwisho wa mazungumzo na walitoa wito kwa wananchi wote wa Congo, viongozi wa dini, na vyombo vya habari kuunga mkono na kusambaza ujumbe wa matumaini na amani.
Tarehe 18 Machi 2025, Emir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, aliwakutanisha Rais wa Rwanda Paul Kagame na Rais wa DRC Félix Tshisekedi katika mazungumzo yaliyolenga kupunguza mvutano wa muda mrefu kati ya mataifa hayo mawili.
Mazungumzo hayo yalifuatwa na ziara ya viongozi wa AFC/M23 nchini Qatar, wakiwemo kiongozi wa kisiasa Bertrand Bisimwa na Kanali Nzenze Imani John, mkuu wa ujasusi na operesheni za kijeshi.
Katika ziara hiyo, serikali ya Qatar iliwauliza maswali wawakilishi wa AFC/M23, ambao walieleza kwa nini walichukua silaha na wanachotaka kutoka kwa serikali ya DRC.
Sasa M23 imeondoa wajumbe wake, wakati ambapo kuna tishio la kurejea kwa mapigano makali kati ya kundi hilo na jeshi la serikali magharibi mwa mkoa wa Kivu Kaskazini.
Hii inakuja baada ya M23 kuwaonya wakazi wa Wilaya ya Walikale wiki hii kwamba huenda wakachukua tena mji wa Pinga, uliopo karibu.




