Kocha kutoka Afghanistan aliyeitwa Ashgar amefariki dunia kwa huzuni kubwa wakati wa kambi ya mafunzo ya watoto iliyokuwa imeandaliwa na Bayern Munich katika jiji la Riesa, Saxony, nchini Ujerumani.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Ujerumani, Ashgar alianguka wakati wa mapumziko ya chakula cha mchana kwenye uwanja wa Feralpi Arena. Japokuwa msaada wa dharura ulifika haraka, alifariki alipofikishwa hospitalini.
Kambi hiyo ilikuwa imewaleta pamoja watoto 119 wa kiume na wa kike kutoka Riesa na maeneo jirani, waliokuwa wakitarajiwa kufundishwa na makocha wa timu maarufu ya Bundesliga.
Katika taarifa rasmi, Bayern Munich ilisema:
“Tuna huzuni kubwa na tuko katika maombolezo mazito. Hakuna maneno ya kueleza haya. Tunawapa pole za dhati familia na marafiki wa Kocha Ashgar.”
Klabu yake kutoka Austria, TSV Hartberg, ambako alikuwa anafundisha timu ya watoto chini ya miaka 13, ilitoa heshima kwenye mitandao ya kijamii, ikisema alikuwa mpendwa sana na wachezaji, wazazi na wafanyakazi kwa sababu ya upole na weledi wake.
Bayern Munich ilisitisha kambi hiyo mapema na kuandaa msaada wa kisaikolojia kwa watoto, wazazi na makocha wote waliokuwepo wakati tukio hilo lilipotokea.




