Jana, Jumanne tarehe 1 Julai 2025, kundi la waasi wa ADF (Allied Democratic Forces) liliwaachilia watu 23 waliokuwa wametekwa nyara katika eneo la Mambasa, mkoa wa Ituri, kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa maafisa wa usalama wa eneo hilo.
Waliyoachiliwa ni pamoja na wanawake na watoto, ambao wote walionekana wakiwa dhaifu sana, baada ya kukaa siku kadhaa matekani ndani ya misitu walikokuwa wakishikiliwa na wapiganaji wa ADF — kundi la waasi linalopinga serikali ya Uganda na ambalo linaendesha shughuli zake kwenye misitu ya mashariki mwa Congo.
Inaripotiwa kuwa mateka hao waliachiliwa kwa hiari na waasi katika eneo la Elake, maarufu kwa mapigano ya mara kwa mara na vitendo vya kikatili vya ADF.
Elake pia linajulikana kwa matukio ya ugaidi, unyang’anyi wa mali za raia, ukatili, na utekaji nyara wa watu.
Tukio hili linatokea baada ya shambulio lingine wiki iliyopita, ambapo waasi wa ADF walivamia tena Elake, wapiganaji wawili wa Maï-Maï waliuawa, mali nyingi za wakazi zikaibiwa, na takriban watu 50 wakatekwa nyara.
Shambulio hilo lilifanya baadhi ya wananchi kujaribu kujilinda wenyewe, lakini ADF waliwashinda kwa nguvu, wakawaua baadhi na kuwajeruhi vibaya wengine.
Viongozi wa eneo la Mambasa wamesema kuwa waasi wa ADF bado wanazunguka kwenye misitu wakiwa na silaha nzito, na takriban raia wengine 20 bado wanashikiliwa mateka.
Waliyoachiliwa wamesema kuwa mateka waliobaki wako kwenye hali mbaya sana, baadhi yao wagonjwa na majeruhi wakihangaika bila huduma yoyote ya afya.
Wananchi wanatoa wito kwa jeshi la FARDC kuchukua hatua ya haraka ili kuwakomboa mateka waliobaki na kulisambaratisha kabisa kundi la ADF kutoka misitu ya Mambasa, ili amani irejee kwa raia wa maeneo hayo.




