Shirika la afya ya umma, Project Access Foundation, limetoa ushauri muhimu wa mambo 10 ya kusaidia watu kujihusisha katika ngono salama, ili kuzuia maambukizi ya magonjwa ya zinaa (STIs) na mimba zisizotarajiwa.
Kwa mujibu wa shirika hilo, vidokezo hivi vina lengo la kulinda afya ya mtu binafsi na mwenza wake, na kusaidia kujenga jamii endelevu inayothamini afya ya uzazi na ngono.
Haya ndiyo maelekezo hayo 10:
Tumia kondomu vizuri kila wakati: Hakikisha unatumia kondomu kwa usahihi kila unapofanya ngono.
Pima afya yako mara kwa mara: Kupima mara kwa mara na kuzungumza wazi na mwenza wako kuhusu hali yako ni muhimu kabla ya kushiriki ngono.
Zungumza kwa uwazi kuhusu afya ya ngono: Mawasiliano ya wazi hujenga uaminifu na huepusha migogoro.
Pata chanjo dhidi ya magonjwa ya zinaa: Chanjo kama HPV, Hepatitis B na Herpes husaidia kuzuia magonjwa yasiyotibika.
Tumia vilainisho vilivyoidhinishwa: Husaidia kupunguza uwezekano wa kondomu kupasuka na kuboresha starehe ya tendo.
Epuka kushirikiana vifaa vya ngono: Ikiwa unatumia sex toys, tumia kondomu na usafishe kabla na baada ya matumizi.
Punguza idadi ya wapenzi wa ngono: Kuwa na wapenzi wengi huongeza hatari ya kuambukizwa magonjwa.
Epuka pombe na dawa za kulevya kabla au wakati wa ngono: Hupunguza uwezo wa kufanya maamuzi sahihi.
Lenga afya yako kwa ujumla: Kula vizuri, lala vya kutosha na punguza msongo wa mawazo ili kuwa na afya bora ya ngono.
Mwona daktari mapema ukihisi kuna tatizo: Ukifanya ngono bila kinga au ukiona dalili fulani, tafuta usaidizi wa matibabu mara moja.




