Kuanzia alfajiri ya Alhamisi, Mei 15, kulitokea mapigano makali kati ya waasi wa M23 na wapiganaji wa Wazalendo katika vijiji kadhaa vya Buabo na Banyungu, vilivyopo katika eneo la Masisi.
Kwa mujibu wa raia walionukuliwa na Radio Okapi, mapigano haya yalianza baada ya shambulio la waasi wa AFC-M23 dhidi ya Wazalendo siku ya Jumatano. Alhamisi, Wazalendo walijibu kwa shambulio la kulipiza kisasi, wakilenga kurejesha maeneo waliyofukuzwa.
Kuanzia saa kumi alfajiri (saa za huko), sauti za silaha nzito na nyepesi zilisikika sana, hasa karibu na milima ya Showa katika eneo la Banyungu, na pia Ngwaki na Lwansihe katika Buabo jirani.
Kwa mujibu wa viongozi wa mitaa, waasi wa M23 walitoka kwenye mji mkuu wa eneo la Masisi, takriban km 12 kaskazini, na wakashambulia ngome muhimu za Wazalendo siku ya Jumatano, wakawafurusha.
Hata hivyo, jaribio la Wazalendo la kurejesha vijiji hivyo siku ya Alhamisi halikufanikiwa.




