Watu wasiopungua 38 wamefariki dunia na wengine 28 kujeruhiwa baada ya mabasi mawili kugongana uso kwa uso na kushika moto katika mkoa wa Kilimanjaro, kaskazini mwa Tanzania.
Mkuu wa mkoa huo, Nurdin Babu, amesema ajali hiyo ilitokea jioni ya Jumamosi katika wilaya ya Same.
Amesema kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya tairi la mbele la moja ya mabasi kulipuka, na kusababisha moto ulioteketeza magari yote mawili, na kuua na kujeruhi abiria wengi waliokuwemo.
Kati ya waliojeruhiwa 28, watu 22 walitibiwa na kuruhusiwa kutoka hospitalini, huku wengine sita wakiendelea kupokea matibabu.
Ajali za barabarani ni jambo la kawaida nchini Tanzania, na mara nyingi husababishwa na magari mabovu na uendeshaji wa kiholela.




