Katika eneo la Shillai, katika jimbo la Himachal Pradesh nchini India, mwanamke aitwaye Sunita Chauhan alifunga ndoa na kaka wawili, Pradeep na Kapil Negi, katika sherehe ya jadi isiyo ya kawaida inayoitwa Jodidara.
Sherehe hiyo ilianza tarehe 12 Julai 2025 katika eneo la Trans-Giri, wilaya ya Sirmaur, na kuhudhuriwa na mamia ya watu kutoka maeneo mbalimbali.
Iliambatana na nyimbo za kitamaduni, ngoma na mila za kale za jamii ya Hatti, kabila la asili lililotambuliwa rasmi kama waliodumaa kiuchumi miaka mitatu iliyopita.
Sunita alisema aliolewa kwa hiari yake bila kulazimishwa, na alitoa shukrani kwa mshikamano wa familia hizo mbili.
Pradeep anafanya kazi serikalini huku Kapil akiwa mfanyakazi wa ng’ambo. Wote wawili walieleza kuwa walichagua kufanya ndoa yao ijulikane kutokana na fahari ya umoja wao na mapenzi ya dhati kwa mke wao wa pamoja.
Kwa mujibu wa wataalamu na viongozi wa tamaduni wa jamii hiyo, aina hii ya ndoa ya kaka kumuoa mke mmoja ilianzishwa ili kuepuka kugawanya ardhi ya kifamilia.
Wakati kaka wanaoa mwanamke mmoja, ardhi haigawanywi, na familia hubaki imara na mali zao hudumu kwa muda mrefu. Ilitumika pia kuimarisha uhusiano wa kifamilia, kulinda usalama wa kaya, na kulima ardhi iliyoko maeneo tofauti.
Katika sherehe iitwayo “Jajda”, bibi harusi hupelekwa nyumbani kwa bwana harusi, anabarikiwa na mtu anayeitwa “Seenj” ambapo kiongozi wa dini ya asili huwasalisha maombi, huwanyunyizia maji matakatifu, na kuwapa sukari ghafi kama ishara ya umoja na mapenzi.
Ingawa desturi hii imeanza kupotea kutokana na maendeleo na elimu, bado inaendelea kufanywa kwa siri au wazi wazi kama ilivyofanywa na Sunita na ndugu wa familia ya Negi.




