Rumeysa Gelgi, mwanamke mrefu zaidi duniani, amefichua kuwa lazima alipe viti sita kwenye ndege kila anaposafiri.
Kwa kawaida, Rumeysa mwenye umri wa miaka 28, ana urefu wa mita 2.15 na anahitaji kulala wakati wote wa safari kwa sababu ya hali yake ya kiafya isiyo ya kawaida.
Rumeysa anatoka katika Wilaya ya Karabük nchini Uturuki na hutumia kiti cha magurudumu au msaada wa kutembea kila siku. Hadi sasa, ni Turkish Airlines pekee inayomwezesha kusafiri kwa ndege kwa kumtoa viti sita na kuweka kifaa maalum cha kumlaza ndani ya ndege.
Alisafiri kwa mara ya kwanza mwezi Septemba mwaka 2022, akitoka San Francisco kwenda California. Tangu wakati huo, Rumeysa ametembelea nchi kama Uhispania, Italia, Marekani, na Uingereza. Hata hivyo, safari zake si rahisi kwani huhitaji kulala muda wote wa safari na kufika uwanja wa ndege saa nne kabla ili ahudumiwe na madaktari.
Ingawa anatamani kutembelea maeneo kama Tokyo, Kyoto, Shanghai na Seoul, ndoto yake kubwa ni kuona maeneo ya kihistoria karibu na nyumbani kwake mjini Safranbolu. Lakini hadi sasa, maeneo hayo hayajatoa mazingira rafiki kwa watu wenye ulemavu kama yeye.
Rumeysa anasema changamoto kubwa anayokutana nayo ni jinsi maeneo mengi hayajazingatia watu wenye ulemavu. Anaongeza kuwa ingawa wafanyakazi wengi huwa na nia njema ya kusaidia, njia wanazotumia mara nyingi huwa si salama vya kutosha.
Alihitimisha kwa kutoa wito wa kubuni njia mpya na za kisasa za kusaidia watu wenye ulemavu kutembelea maeneo ya kihistoria, kwa sababu kila mtu anastahili nafasi ya kuifahamu historia na uzuri wa dunia.
Rumeysa ana ugonjwa adimu uitwao Weaver Syndrome ambao husababisha ukuaji wa kupita kiasi kuliko watu wengine.





