Ndege ya kijeshi ya Uganda ilianguka asubuhi ya Jumanne, Julai 2, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Aden Adde, uliopo mjini Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.
Mamlaka ya usafiri wa anga ya Somalia imethibitisha kuwa ndege hiyo ilikuwa na abiria wanane na ilikuwa imetokea kituo cha kijeshi cha Balidogle, katika eneo la Lower Shabelle.
Ripoti kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa ndege hiyo ililipuka na kushika moto mara tu baada ya kutua, lakini vikosi vya dharura vilifika haraka na kuuzima moto kabla haujasababisha madhara makubwa.
Mashuhuda walisema walisikia mlipuko mkubwa kisha kuona moshi mzito mweusi ukipaa juu ya eneo la ajali.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Somalia, Ahmed Maalim, aliambia BBC kuwa ajali hiyo ilitokea kwenye eneo la kijeshi la uwanja huo na kwamba uchunguzi umeanzishwa ili kubaini chanzo cha ajali. Hakuna taarifa rasmi kuhusu vifo au majeruhi zilizotolewa kufikia sasa.
Wanajeshi wa Uganda wako Somalia kama sehemu ya ATMIS – Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia, wakishirikiana na jeshi la serikali ya Somalia katika vita dhidi ya kundi la kigaidi la al-Shabab, ambalo limekuwa likipigana kwa miaka kadhaa.




