Ngũgĩ wa Thiong’o, mwandishi mashuhuri wa Kenya anayejulikana duniani kwa kazi zake za fasihi zilizolenga kukosoa ukoloni na athari zake kwa bara la Afrika, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 87.
Binti yake, Wanjiku wa Ngũgĩ, alitangaza kifo chake kupitia Facebook, akisema: “Ameishi maisha mazuri, amepigana vita nzuri.”
Ngũgĩ alifariki dunia Jumatano asubuhi jijini Atlanta, Marekani. Taarifa zaidi kuhusu kifo chake zitatolewa katika siku zijazo.
Ngũgĩ alizaliwa katika familia ya wakulima wakati wa utawala wa kikoloni wa Waingereza nchini Kenya. Alipata umaarufu kimataifa kupitia kazi zake mashuhuri kama Weep Not, Child (1964), Devil on the Cross (1980), na Wizard of the Crow (2006).
Alikuwa miongoni mwa waandishi wachache waliamua kuandika kwa lugha yao ya mama—Kikuyu—kama njia ya ukombozi wa kiutamaduni.
Aliwahi kusema: “Ni gerezani nilipoanza kufikiria kwa kina kuhusu lugha. Kwa nini sikuwa nimezuiwa kabla wakati niliandika kwa Kiingereza?”
Mnamo mwaka 1977, alifungwa gerezani baada ya kuandika na kuigiza tamthilia Ngaahika Ndeenda (Nitaoa Nitakapotaka), iliyoandikwa kwa Kikuyu. Tamthilia hiyo ilikosoa ukosefu wa usawa wa kiuchumi na unafiki wa kidini, na hivyo kuvuruga utawala wa Rais Daniel arap Moi.
Baada ya kuachiliwa mwaka 1978, alikimbilia uhamishoni Uingereza kisha Marekani, ambako alifundisha katika Chuo Kikuu cha California, Irvine.
Mwaka 2004, alipoamua kurudi Kenya, yeye na mke wake Njeeri walivamiwa na watu wenye silaha nyumbani kwao.
Ngũgĩ aliendelea kuwa mtetezi thabiti wa lugha na tamaduni za Kiafrika, akisisitiza kuwa lugha za kigeni hazipaswi kutawala mfumo wa elimu au maonyesho ya utamaduni.
Wakati akifundisha katika Chuo Kikuu cha Nairobi, alisisitiza: “Fasihi ya Kiafrika lazima iwe mstari wa mbele ili mataifa na tamaduni nyingine zijifunze kutoka kwetu.”
Mnamo mwaka 2021, Ngũgĩ aliteuliwa kuwania tuzo ya International Booker Prize kupitia kazi yake ya kishairi The Perfect Nine, iliyokuwa kazi ya kwanza kutuma kwa lugha ya asili ya Kiafrika.
Zaidi ya kuwa msomi na mwandishi, Ngũgĩ alikuwa baba wa watoto tisa. Watoto wanne kati yao—Tee Ngũgĩ, Mukoma wa Ngũgĩ, Nducu wa Ngũgĩ, na Wanjiku wa Ngũgĩ—walifuata nyayo zake za kifasihi.
Katika mahojiano na The Guardian mwaka 2018, alisema: “Kupinga dhuluma ni njia bora ya kuendelea kuishi. Hata kama ni kitendo kidogo tu, kusema ‘hapana’ kwa uovu ni ushindi.”
Ngũgĩ wa Thiong’o ameacha urithi mkubwa wa kupigania lugha, tamaduni, na haki za Waafrika kupitia maandiko na mafundisho yake.
Atakumbukwa milele kama nguzo ya fasihi na utambulisho wa Afrika ya kisasa.




