Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Léon XIV, ametoa wito wa kusitishwa kwa vita vinavyoendelea huko Gaza, akisema vinaendelea kuua watu wengi, hasa raia wa kawaida.
Vita vya Gaza vimekuwa kati ya Jeshi la Israel na kikundi cha Hamas. Hivi karibuni, jeshi la Israel lilishambulia kanisa lililoko katika eneo la Gaza, ambapo watu watatu waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa.
Wakati wa kumalizia sala ya Malaika wa Bwana (Angelus), Jumapili hii ya tarehe 20 Julai 2025, Papa Léon XIV alizungumzia huzuni yake kutokana na mashambulizi hayo ya Israeli kwenye kanisa, na kutaka vita hivyo vikome kwa kuwa vimesababisha vifo vingi vya watu wasio na hatia.
Papa Léon XIV alisema:
“Ninarudia tena ombi langu kwamba vita hivi vikome ili amani irejee katika eneo hili.”
Shambulio hilo la kanisa limeibua msimamo mkali kutoka kwa Vatikani, kwani watu watatu waliuawa na wengi kujeruhiwa, wakiwemo padri aliyekuwa kiongozi wa kanisa hilo.
Kwa upande wake, Israel ilisema kuwa tukio hilo lilikuwa ajali na halikulengwa makusudi. Pia ilitangaza kwamba uchunguzi umeanzishwa kuhusu tukio hilo.




