arton133211

Rwanda Yakanusha FDLR Kuwapo Katika Maeneo Yanayodhibitiwa na M23

Serikali ya Rwanda imekanusha madai kwamba wapiganaji wa FDLR wapo katika maeneo yanayodhibitiwa na kundi la waasi la M23, ikieleza kuwa hilo haliwezekani kwa kuwa wapiganaji hao tayari wameingizwa katika jeshi la taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC).

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Balozi Olivier Nduhungirehe, katika mahojiano na gazeti la Jeune Afrique.

Mahojiano hayo yalifuata makubaliano ya amani yaliyosainiwa wiki iliyopita kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwa upatanishi wa Marekani.

Moja ya vipengele vya makubaliano hayo ni kwamba serikali ya DRC inapaswa kulivunja kundi la waasi la FDLR, na hatua hiyo ifuatiwe na Rwanda kuondoa “hatua zake za kujihami.”

Waziri Olivier Nduhungirehe alisisitiza kuwa FDLR ni lazima livunjwe, hasa kwa kuwa hata serikali ya DRC inakubali kwamba ni tatizo—licha ya kulijumuisha katika jeshi lake rasmi.

Alisema: “FDLR linaungwa mkono na serikali ya Congo, na hata limeingizwa kwenye FARDC. Ripoti za Umoja wa Mataifa zinalithibitisha hilo. Si Rwanda pekee inayolisema… ni lazima FDLR livunjwe. Serikali ya DRC inakubali kuwa FDLR ni tatizo linalopaswa kushughulikiwa, jambo litakalosaidia Rwanda kuondoa hatua zake za kujihami.”

Hata hivyo, Waziri Nduhungirehe alikanusha vikali madai kwamba FDLR iko katika maeneo ya M23, hasa katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Alisema: “FDLR haipo katika maeneo yanayodhibitiwa na M23, kwa sababu FDLR tayari imeingizwa katika jeshi la Congo na inashirikiana na wanajeshi wa Congo.”

“Atawezaje mtu kusema FDLR iko kwenye maeneo ya M23? FDLR inafanya kazi na FARDC. Je, FARDC iko kwenye maeneo ya M23? Hapana. Kwa sababu FDLR ni sehemu ya FARDC na wanashirikiana. Kwa hiyo kusema kwamba FDLR iko kwenye maeneo ya M23 sina uhakika mna maana gani.”

Alipoulizwa kuhusu mahali walipo sasa wapiganaji wa FDLR, Waziri Nduhungirehe alisema kuwa hilo si jukumu la wizara yake, bali litashughulikiwa na kamati ya pamoja ya ujasusi kati ya majeshi ya Rwanda na DRC.

Msemaji wa Jeshi la Rwanda, Brigedia Jenerali Ronald Rwivanga, alitangaza hivi karibuni kwamba FDLR lina wapiganaji kati ya 7,000 na 10,000, walioko katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini, pamoja na msitu wa Kibira nchini Burundi.

Sangiza iyi nkuru

Soma Izindi Nkuru

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *