Ukraine imefanya shambulio kubwa la drone katika kiwanda cha kijeshi kilichopo Izhevsk, katikati mwa Urusi, umbali wa zaidi ya kilomita 1,000 kutoka mpaka wa Ukraine.
Kiwanda hicho, kiitwacho Kupol Electromechanical Plant, huzalisha makombora ya Tor, rada na silaha za ulinzi wa anga.
Shambulio hilo limesababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi wengine 45, wakiwemo sita waliopata majeraha mabaya, kwa mujibu wa mamlaka ya mkoa wa Udmurtia.
Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha milipuko juu ya majengo ya kiwanda hicho, ikifuatiwa na moshi mzito.
Shirika la Usalama la Ukraine (SBU) limedai kuhusika, likisema kuwa drones mbili zilipita umbali wa km 1,300 ili kufikia kiwanda hicho. Lengo lilikuwa kupunguza uwezo wa kiwanda hicho kuzalisha silaha na kuonyesha kwamba hakuna miundombinu ya kijeshi salama ndani ya Urusi.
Hii ni mara ya pili kwa kiwanda hicho kushambuliwa tangu Novemba, ingawa shambulio la awali halikusababisha vifo.
Wakati Ukraine ilifanya shambulio hilo, Urusi nayo ilishambulia kwa kufyatua makombora 537 dhidi ya Ukraine mwishoni mwa wiki, ikiathiri maeneo kama Kyiv na Lviv.




