Wanajeshi wa makundi ya Wazalendo, wanaoshirikiana na jeshi la serikali ya Congo kupambana na waasi wa M23, waligongana wao kwa wao siku ya Ijumaa, tarehe 16 Mei, na kusababisha vifo vya wapiganaji wawili.
Mapigano yalizuka asubuhi ya Ijumaa kati ya makundi kutoka Kivu Kusini na Kivu Kaskazini, katika eneo moja ndani ya Wilaya ya Fizi, mkoani Kivu Kusini.
Mapambano hayo yalitokea katika kijiji cha Malicha/Simbi, karibu sana na mji wa Baraka, mji mkubwa zaidi katika wilaya hiyo.
Taarifa kutoka eneo hilo zinasema kwamba mapigano hayo, yanayohusishwa na kundi la Yakutumba, yalisababisha vifo vya wapiganaji wawili wa Wazalendo na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Si mara ya kwanza kwa Wazalendo kugombana wao kwa wao katika maeneo kama Fizi na Uvira. Miezi miwili iliyopita, wanachama wa makundi ya Hamuri Yakutumba na Ebwira Mutetezi Trésor walirushiana risasi na hatimaye Trésor kuuawa.
Katika Uvira, migogoro ya ndani ni ya kila siku, hasa kati ya vikundi vinavyoongozwa na Gashumba, Makanaki John, na Rene.




