Vyombo vya habari katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) vimepigwa marufuku kuripoti kuhusu Rais wa zamani Joseph Kabila au kutoa taarifa na maelezo yoyote kuhusu shughuli za chama chake cha siasa, PPRD (Chama cha Watu wa Ujenzi na Demokrasia).
Siku ya Jumanne, tarehe 3 Juni, Christian Bosembe, Rais wa Baraza Kuu la Mawasiliano ya Habari (CSAC), alitangaza uamuzi huo kupitia kituo huru cha redio Top Congo.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, vyombo vya habari vya taifa haviruhusiwi tena kuripoti au kuonyesha taarifa zozote kuhusu PPRD, wala kupeperusha mahojiano au kauli zozote za kiongozi wake, Joseph Kabila.
Christian Bosembe alieleza:
“Hii si censure. Hakuna haki iliyokiukwa. Televisheni haitakiwi kutumika kama jukwaa la kupindua serikali.”
Hatua hii imechukuliwa baada ya Seneti ya DRC kumuondolea Joseph Kabila kinga ya kisiasa, siku ya Alhamisi, tarehe 22 Mei, kufuatia kupitishwa kwa ripoti ya kamati maalum iliyochunguza tuhuma zilizowasilishwa na Mkaguzi Mkuu wa Serikali kwa Mahakama ya Juu ya Kijeshi.
Kwa sasa, Joseph Kabila anakabiliwa na mashtaka, ikiwemo makosa ya kivita na madai ya kushirikiana na kundi la waasi la AFC/M23.




