Kundi la waasi wa M23 limeanza kuukaribia mji wa Uvira, mji wa pili kwa ukubwa katika jimbo la Kivu Kusini, hali inayozua hofu kuwa mji huo unaweza kutwaliwa na waasi.
Tangu Alhamisi, vikosi vya M23 vimeonekana katika maeneo yanayouzunguka mji huo, ikiwemo Katogota na Luvungi. Taarifa za Ijumaa zinaonyesha kuwa wanajeshi wa M23 wanaendelea kusonga mbele wakizunguka Uvira.
Uvira, ulio kando ya Ziwa Tanganyika, umekuwa ukilindwa tangu Februari na majeshi ya serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (FARDC), wanajeshi wa Burundi, pamoja na wapiganaji wa makundi ya Wazalendo. Vikosi hivyo vilijificha Uvira baada ya kushindwa na M23 na kutimuliwa katika mji mkuu wa jimbo, Bukavu.
Kusonga kwa M23 kuelekea Uvira kunatokea wakati mazungumzo ya amani yakiendelea mjini Doha, Qatar, kati ya waasi na serikali ya Kinshasa, kwa lengo la kumaliza mgogoro ambao umedumu kwa zaidi ya miaka mitatu.




