Wanajeshi wa Burundi walioko nchini Rwanda wameungana na Jeshi la Rwanda (RDF) pamoja na Polisi ya Taifa ya Rwanda kutoa msaada kwa familia zisizojiweza.
Burundi ni miongoni mwa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yaliyopeleka majeshi Rwanda kwa ajili ya kushiriki kwenye Wiki ya tano ya CIMIC ya EAC, inayolenga maendeleo ya jamii.
Matukio ya Wiki ya CIMIC yalianza tarehe 29 Juni na yatamalizika Alhamisi, tarehe 3 Julai 2025, yakilenga kusaidia wananchi wa Rwanda kusherehekea Siku ya Ukombozi kwa vitendo vya mshikamano.
Kwa mujibu wa ukurasa rasmi wa X wa Jeshi la Burundi, wanajeshi wake walikabidhi vifaa muhimu kwa familia 70 zisizo na uwezo katika maeneo mbalimbali nchini Rwanda.
Vifaa hivyo ni pamoja na vitanda, magodoro, mashuka, viti vya nyumbani na meza.
Familia hizi ziko katika wilaya za Nyarugenge, Musanze, Burera, Nyagatare, Ngororero, Karongi, na Nyanza.
Mbali na msaada huu kwa familia masikini na miradi ya miundombinu, madaktari bingwa kutoka majeshi ya EAC pia wanatoa huduma za afya bila malipo kwa wananchi wa Rwanda.
Huduma hizo zinajumuisha matibabu ya ndani ya mwili, afya ya wanawake, watoto, mifupa, meno, na mengineyo.
Huduma hizi zinapatikana katika hospitali za wilaya za Ngoma na Nyanza.




