Utafiti uliofanywa katika vituo sita vya IVF nchini Hispania na Italia umeonesha kuwa wanaume walio na umri wa zaidi ya miaka 45 wanaweza kuwa kikwazo kikubwa katika uzazi, hata pale ambapo mayai ya wanawake wachanga yanatumika.
Uchunguzi huo ulihusisha mizunguko 1,712 ya upandikizaji kati ya mwaka 2019 hadi 2023, ambapo umri wa wastani wa wanawake ulikuwa miaka 26, na wanaume waligawanywa kati ya wale walio chini au zaidi ya miaka 45.
Ingawa viwango vya urutubishaji na ukuaji wa kiinitete vilikuwa sawa katika makundi yote mawili, hatari ya mimba kuharibika ilikuwa juu kwa wanaume waliovuka miaka 45 (23.8%), ukilinganisha na wanaume wa chini ya miaka 45 (16.3%).
Zaidi ya hayo, idadi ya watoto waliozaliwa salama ilikuwa chini kwa wanaume wakubwa (35.1%) ikilinganishwa na wale vijana (41%).
Dkt Maria Cristina Guglielmo, mtaalamu wa biolojia ya seli za uzazi, amesema kuwa umefika wakati madaktari waanze kuzingatia umri wa wanaume kama kipengele muhimu cha uzazi, kama ilivyo kwa wanawake.
Aliongeza kuwa kadri mwanaume anavyozeeka, mbegu zake za kiume huweza kuwa na hitilafu za DNA, jambo linaloweza kuharibu kiinitete au kusababisha mimba kuharibika.
Utafiti huu unatoa wito kwa vituo vya afya ya uzazi kuwapa watu wote wawili taarifa kamili, kwani umri wa mwanaume unaweza pia kuathiri uwezo wa kupata watoto, sawa na ule wa mwanamke.




