Mtaalamu wa afya, Dkt. Iyayi Osifo kutoka Nigeria, ametangaza kuwa kuna watu wenye mabadiliko ya kipekee ya kijeni yanayowafanya wasiweze kuambukizwa na virusi vya UKIMWI (VVU).
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Dkt. Osifo alisema kuwa watu hao wana mabadiliko maalum katika seli zao, hasa kwenye kipengele kinachoitwa CCR5 receptor, ambacho VVU hutumia kuingia ndani ya seli za mwili. Ikiwa mtu hana CCR5, virusi haviwezi kuingia, na hivyo haviwezi kuambukiza.
Akasema:
“Wapo watu wanaweza kushiriki ngono bila kinga na mtu mwenye VVU lakini wasipate maambukizi, kwa sababu ya muundo wao maalum wa kijeni.”
Dkt. Osifo aliongeza kuwa mabadiliko haya yanapatikana zaidi kwa watu kutoka Ulaya ya Kaskazini, lakini pia yamewahi kugunduliwa – ingawa kwa nadra sana – kwa watu kutoka Nigeria, Ghana, na Kenya.
Hata hivyo, alionya dhidi ya kutegemea kinga hiyo ya asili.
“Hii ni kinga ya kipekee na nadra sana. Haitakiwi kutumiwa kama sababu ya kuwa na uzembe au kushiriki ngono bila kinga.”
Aliwatia moyo pia wale wanaoishi na VVU, akisema kuwa kuna dawa za kisasa zinazowawezesha kuishi maisha ya kawaida, hasa iwapo watagunduliwa mapema na kuanza tiba haraka.
“Ukijua hali yako mapema na kuanza dawa kwa wakati, unaweza kuishi kama watu wengine wote.”




