d7fb1c30-b6ec-11ef-a2ca-e99d0c9a24e3

Zambia: Familia ya Rais wa Zamani Lungu Yasitisha Kurudisha Mwili Wake Kutoka Afrika Kusini

Familia ya aliyekuwa Rais wa Zambia, Edgar Lungu, imesitisha kurejeshwa kwa mwili wake kutoka Afrika Kusini, ikidai kuwa serikali haijatekeleza makubaliano muhimu kuhusu mazishi yake.

Mipango ilikuwa imekamilika, na mwili wake ulitarajiwa kurejeshwa Jumatano iliyopita kwa ndege ya kukodi, baada ya majadiliano ya muda mrefu kati ya familia na serikali.

Hata hivyo, familia imesitisha mpango huo, ikisema kuwa sasa ni “vigumu sana kuamini kuwa serikali itaheshimu makubaliano waliyoafikiana.”

Makebi Zulu, msemaji wa familia, alisema Jumatano: “Cha kusikitisha ni kwamba mabaki ya Rais Edgar Chagwa Lungu hayatarejea leo.”

Zulu alisema kuwa serikali ilitoa ratiba ya mazishi bila kushauriana na familia, kama ilivyoripotiwa na BBC.

Ilikuwa imepangwa kuwa Rais Hakainde Hichilema angepokea mwili huo pindi utakapowasili uwanja wa ndege wa Lusaka.

Mwili huo ulitarajiwa kupelekwa nyumbani kwake Lusaka, ambapo sherehe ya kumuaga ilikuwa imepangwa kwa tarehe 22 Juni, kisha azikwe siku inayofuata.

Akizungumza akiwa Afrika Kusini, Zulu alisema serikali imekiuka makubaliano ya awali.

Akiwa ameandamana na jamaa wa karibu, alisema: “Tunatumaini siku moja mwili wake utarejeshwa nyumbani na kupewa mazishi ya heshima.”

Serikali haijatoa tamko rasmi.

Hii ni mara ya pili familia kuzuia kurudishwa kwa mwili huo kutokana na mzozo unaozidi kuongezeka kuhusu nani anapaswa kusimamia mazishi.

Chama cha upinzani cha PF, ambacho Lungu alikuwa anakiongoza hadi alipofariki, kimeunga mkono msimamo wa familia na kuituhumu serikali kwa kutaka kutumia maombolezo kwa maslahi ya kisiasa.

Lungu, aliyekuwa rais wa Zambia kuanzia 2015 hadi 2021, alifariki mwanzo wa mwezi huu akiwa Afrika Kusini alipokuwa akipokea matibabu ya ugonjwa ambao haukujulikana wazi. Zambia kwa sasa inaendelea kuomboleza kwa siku 16 za maombolezo ya kitaifa.

Sangiza iyi nkuru

Soma Izindi Nkuru

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *